Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) Limetangaza matokeo ya uchaguzi wa awamu ya kwanza kwa waombaji wa programu za Afya na Sayansi Shirikishi kwa mwaka wa masomo 2025/2026 .
Baraza liliratibu udahili wa wanafunzi katika kozi mbalimbali za afya na sayansi shirikishi kupitia Mfumo wa Udahili wa Pamoja (CAS) kwa mwaka wa masomo 2025/2026. Jumla ya waombaji 33,986 waliwasilisha maombi yao kupitia CAS. Jumla ya waombaji 27,785 walikamilisha maombi yao kwa kuchagua vyuo/programu walizozipenda. Jumla ya waombaji 25,515 walikuwa na sifa kwenye programu walizoomba na jumla ya waombaji 2,270 hawakuwa na sifa kwenye programu walizoomba.
Jumla ya waombaji 21,565 wamechaguliwa kujiunga kwenye vyuo vinavyotoa programu mbalimbali za Afya na Sayansi Shirikishi ambapo wanawake ni 11,013 (51%) na wanaume 10,552 (49%). Waombaji 4,733 walichaguliwa kwenye vyuo vya serikali na waombaji 16,832 katika vyuo visivyo vya serikali.
Aidha, waombaji wenye sifa ambao hawakuchaguliwa kutokana na ushindani katika programu na vyuo walivyoomba, wanashauriwa kuomba kujiunga katika vyuo vyenye nafasi katika dirisha la awamu ya pili kupitia Mfumo wa Udahili wa Pamoja.
Waombaji wote wanaweza kuangalia matokeo ya uchaguzi kupitia tovuti ya Baraza (www.nactvet.go.tz) kwa kubonyeza CAS Selection 2025 kwa ajili ya kupata taarifa zaidi.
Baraza linautaarifu umma kuwa dirisha la awamu ya pili limefunguliwa rasmi leo tarehe 25/07/2025 hadi tarehe 24/08/2025 na matokeo ya uchaguzi yatatolewa tarehe 01/09/2025.
Aidha, wale wanaohitaji kubadilisha programu au chuo, dirisha la uhamisho litakuwa wazi kuanzia tarehe 25/07/2025 hadi tarehe 24/08/2025, hivyo watumie dirisha hili kukamilisha maombi hayo kupitia tovuti ya Baraza kwa kubonyeza kwenye akaunti yake aliyotumia kuomba na kuchaguliwa.
IMETOLEWA NA: OFISI YA KATIBU MTENDAJI BARAZA LA TAIFA LA ELIMU YA UFUNDI NA MAFUNZO YA UFUNDI STADI (NACTVET)