Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta) limetangaza matokeo ya upimaji wa kitaifa wa darasa la nne kwa mwaka 2024, yakionesha mafanikio makubwa kwa wanafunzi ambapo wasichana wametia fora zaidi ukilinganisha na wavulana. Matokeo haya yalitolewa mapema leo Januari 4, 2025, na Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Said Mohamed, katika mkutano na waandishi wa habari.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa, jumla ya wanafunzi 1,320,227 kati ya 1,530,805 wamefaulu mtihani huo, sawa na asilimia 86.24 ya waliofanya mtihani. Hii ni ongezeko la asilimia 2.9 ikilinganishwa na mwaka 2023 ambapo asilimia 83.34 ya wanafunzi walifaulu. Ufaulu huu unajumuisha wanafunzi waliopata madaraja A, B, C na D, ambao sasa wanatarajiwa kuendelea na masomo yao ya darasa la tano mwaka 2025.
Dk Mohamed amebainisha kwamba kati ya wanafunzi waliofaulu, wasichana wameongoza kwa kufaulu zaidi, ambapo 699,901 wa wasichana sawa na asilimia 87.75 wamefaulu, huku wavulana waliofaulu wakiwa 620,326 sawa na asilimia 84.61. Hii inaonesha jinsi gani jitihada za kuboresha elimu kwa mtoto wa kike zimeanza kuzaa matunda.
Ufaulu huu umepongezwa na wadau mbalimbali wa elimu nchini, hasa ikizingatiwa kwamba maboresho katika mfumo wa elimu na mikakati ya kuwainua wanafunzi hasa katika masomo ya sayansi na hisabati yameangaziwa zaidi katika miaka ya hivi karibuni.
Pamoja na matokeo ya darasa la nne, Dk Mohamed pia ametangaza matokeo ya kidato cha pili, ambapo wavulana wakiongoza kwa ufaulu. Wanafunzi 680,574 kati ya 796,825 wamefaulu, sawa na asilimia 85.41. Hii ni ongezeko dogo la asilimia 0.1 ikilinganishwa na mwaka 2023. Katika idadi hiyo, wanafunzi wa kiume waliofaulu ni 313,117 wakati wasichana ni 367,457.
Matokeo haya yanaashiria mwanzo mzuri kwa mwaka wa kitaaluma wa 2025, na yanatoa matumaini kwa mwelekeo mzuri wa kiwango cha elimu nchini Tanzania. Serikali, kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, pamoja na wadau wengine, wana kila sababu ya kuendeleza jitihada zao katika kuboresha elimu ili kila mtoto aweze kupata fursa sawa ya kujifunza na kujiendeleza.
unaweza kuangalia matokeo ya darasa la nne kupitia linki zifuatazo