Matokeo ya Upimaji wa Kitaifa wa Kidato cha Pili (FTNA) kwa mwaka 2024 yametangazwa na Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA), yakionyesha ongezeko dogo la ufaulu ikilinganishwa na mwaka uliopita. Katibu Mtendaji wa NECTA, Dk. Said Mohamed, aliyatangaza matokeo hayo katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika mkoani Dar es Salaam. Mwaka huu, wanafunzi 680,574 kati ya 796,825 wamefaulu mtihani huo, sawa na asilimia 85.41 ya waliofanya mtihani.
Wavulana wameongoza katika ufaulu huu ambapo asilimia 87.13 ya wavulana waliofanya mtihani wamefaulu, huku wasichana wakiwa na ufaulu wa asilimia 83.99. Hata hivyo, licha ya uongozi wa wavulana kwa jumla, wasichana wameendelea kuonyesha uwezo mkubwa katika baadhi ya masomo.
NECTA pia ilibainisha kuwa imechukua hatua kali dhidi ya udanganyifu ambao bado unajitokeza katika vituo vichache vya mitihani. Matokeo ya wanafunzi 46 yalifutwa kutokana na udanganyifu na vitendo visivyofaa; 41 kati yao walibainika kudanganya wakati watano walipatikana wakiandika matusi katika karatasi zao za majibu. Kituo cha shule ya sekondari Good Will kilichoko Arusha kilifungiwa kuwa kituo cha mitihani kama sehemu ya adhabu dhidi ya vitendo vya udanganyifu vilivyofanyika.
Matokeo haya yametolewa wakati ambapo sekta ya elimu inaendelea kupitia mabadiliko na maboresho yaliyolenga kuboresha viwango vya elimu nchini. Kulingana na Dk. Mohamed, jitihada za kuelimisha jamii pamoja na wasimamizi wa mitihani zimechangia kupungua kwa matukio ya udanganyifu. Aidha, NECTA imesisitiza kwamba itaendelea kuchukua hatua kali dhidi ya wote watakaobainika kuhusika na udanganyifu wa mitihani.
Kwa upande mwingine, matokeo ya kidato cha pili yamekuja yakiwa na maboresho katika masomo ya sayansi na hisabati, ikionekana kuwa jitihada za kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji katika masomo haya zimeanza kuzaa matunda. Hata hivyo, bado kuna changamoto kwenye baadhi ya masomo ya lugha na sanaa ambapo ufaulu umeshuka ikilinganishwa na mwaka uliopita.
Wazazi na walezi wametakiwa kuendelea kushirikiana na shule na walimu katika kuwajengea wanafunzi mazingira mazuri ya kujifunza, sambamba na kuwapatia motisha na mwongozo unaofaa, ili kuendelea kukuza ufaulu na ubora wa elimu nchini. Wakati huo huo, wanafunzi wamehimizwa kuzingatia umuhimu wa kujiamini na kujituma katika masomo yao, kwani mafanikio yao ya kitaaluma yana mchango mkubwa kwa maisha yao ya baadaye.
Unaweza kuangalia matokeo hayo kupitia linki zifuatazo hapo chini
FORM TWO NATIONAL ASSESSMENT (FTNA) 2024 RESULTS ENQUIRIES
Unaweza pia kutumia linki hii hapa: NECTA Form Two Results 2024 link 02