Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) linautaarifu umma kuwa matokeo ya uhakiki wa waombaji waliochaguliwa kujiunga na masomo kwa mkupuo wa Machi, 2025 katika ngazi ya Astashahada na Stashahada yametoka rasmi tarehe 2 Aprili, 2025.
Jumla ya waombaji 10,684 kati yao wanawake 5,325 (49.8%) na wanaume 5,359 (50.2%) waliwasilishwa kwa ajili ya uhakiki kutoka katika vyuo vilivyokidhi vigezo vya kudahili katika mkupuo huu. Kati yao, waombaji 10,419 (98%) (Wanawake 5,197 na Wanaume 5,222), walikuwa na sifa za kujiunga na programu walizoomba, na waombaji 265 (2%) hawakuwa na sifa katika programu walizoomba.
JINSI YA KUANGALIA MATOKEO YA UHAKIKI WA WANAFUNZI WALIOCHAGULIWA KATIKA MKUPUO WA MACHI 2025/2026
Waombaji wote walioomba kujiunga katika programu mbalimbali wanaweza kupata taarifa zao za uhakiki kwa kutumia misimbo iliyotumwa kwenye namba zao simu kwa kubonyeza kitufe cha“Angalia Hali ya Uhakiki wa muhula wa Machi 2025/2026” au kwa kubonyeza kitufe “Uhakiki mkupuo wa Machi, 2025/2026” katika tovuti ya Baraza www.nactvet.go.tz. Baraza linawasisitiza waombaji wote kutunza misimbo watakayotumiwa kwani ndio itatumika katika udahili mara wafikapo chuoni.
Baraza linavielekeza vyuo kuwasajili wanafunzi wenye sifa na watakaowasili vyuoni kwa ajili ya kuanza masomo kuanzia tarehe 7 Aprili, 2025; na kwa kutumia misimbo itakayotumwa na Baraza kwenye namba za simu za waombaji. Hatua stahiki zitachukuliwa dhidi ya chuo kitakachokiuka taratibu za udahili.
Aidha, vyuo vimepewa nafasi ya kurekebisha na kuwasilisha taarifa za waombaji ambazo hazikuwa sahihi kuanzia leo tarehe 3 hadi 7 Aprili, 2025.